Wednesday, December 15, 2010

Zitto

SIKU tatu baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kupima mwenyewe kama aendelee na wadhifa wake wa naibu kiongozi wa upinzani bungeni au aachie ngazi, mbunge huyo amesema kwa sasa anataka kukaa mbali na vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Zitto, uamuzi wake huo unalenga kuepusha mzozo ndani ya chama na kwamba, hata wananchi hivi sasa hawataki kusikia mizozo ikiendelea ndani ya vyama.

“Sina lolote la kusema kwa sasa, I am stay out of media (nataka kukaa mbali na vyombo vya habari), kwa sasa ninachoweza kusema no comment, (sina cha kusema),” alsema Zitto na kuongeza:
“Jambo lolote nitakalosema sasa hivi, litaendelea kukivuruga chama, bora nikae kimia, nadhani hilo litakisaidia zaidi chama.”

Zitto ambaye amejijengea umaarufu kwenye Bunge, amekumbwa na matatizo baada ya kupinga hadharani msimamo wa wabunge wa Chadema kutoka ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete, alipoanza hotuba ya uzinduzi wa Bunge la Kumi.
Mbunge huyo hakuingia ukumbini kutekeleza uamuzi wa wenzake, aliitisha mkutano na waandishi wa habari baada ya kitendo hicho na kutamka kuwa, wabunge wa Chadema hawakupaswa kutoka ukumbini na kuweka bayana jinsi uamuzi huo ulivyofikiwa ndani ya vikao vya wabunge wa Chadema.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alisema chama hakiwezi kuwaachia viongozi wake kufanya mambo yaliyo kinyume na misimamo ya chama, hivyo kimempa fursa Zitto apime mwenyewe kama anaweza kuendelea kuongoza watu wasiokuwa na imani naye.

Dk Slaa alikuwa akizungumzia yaliyojiri kwenye kikao cha wabunge kilichofanyika mjini Bagamoyo wiki iliyopita na kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye mbunge huyo kwa nafasi ya Naibu Kiongozi Kambi ya Upinzani.
Dk Slaa alisema uamuzi wa wabunge wa kutokuwa na imani naye kwa nafasi ya naibu kiongozi bungeni, ulifikishwa kwenye Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Desemba 11, mwaka huu.

“Kamati kuu haikukutana kujadili suala za Zitto, kwa sababu chama hakina mamlaka ya kuingilia kazi ya kamati ya wabunge, bali kilipokea taarifa ya uamuzi wa wabunge hao,” alisema Dk Slaa.
Alisema kutokana na chama kutokuwa na uwezo wa kutoa uamuzi dhidi ya msimamo huo wa kamati ya wabunge, ni jukumu la Zitto mwenyewe kupima uzito na kuchukua uamuzi wa kujiuzulu au kuendelea na wadhifa wake.

No comments: