Tuesday, December 21, 2010

Watu sita wateketea kwa moto Mbeya.

Watu sita wameteketea kwa moto na wengine Kumi na Mmoja wamejeruhiwa baada ya gari aina ya Land Rover walilokuwa wakisafiria kupinduka na kushika moto katika eneo la Kimondo mkoani Mbeya.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya - Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema gari hilo lenye namba za usajili T 491 AFP lilikuwa linatokea mkoani Mbeya kuelekea Makete mkoani Iringa na lilipinduka baada ya kushindwa kupanda mlima.

Amesema jeshi la polisi mkoani Mbeya linaendelea na uchunguzi kufahamu chanzo cha ajali hiyo na kwamba watakapokamilisha uchunguzi huo litatoa taarifa kamili.

Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambapo Daktari wa zamu wa hospitali hiyo, Dominick Chalu amesema baadhi ya majeruhi hao walifikishwa hospitalini hapo hali zao zikiwa ni mbaya.

Akizungumza kwa shida hospitalini hapo, mmoja wa majeruhi hao Okaka Matamsi, alisema gari hilo aina ya Land Rover liliteketea kwa moto lote.
“Tulikuwepo abiria 20; unajua baada ya gari kupinduka huenda kusingekuwa na madhara makubwa, lakini… watu wamekufa na kuungua kutokana na ile petroli iliyokuwa juu ya keria kulipuka na gari zima kushika moto,” alisema Matamsi.

Hosea Cheyo, Mbeya

No comments: