Monday, November 8, 2010

Ziwa Tanganyika laua watano, 21 waokolewa

WATU watano wakiwemo watoto wanne wamefariki dunia na wengine zaidi ya 10
Hawajulikani walipo baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama katika Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Habari za uhakika zilizopatika jana kutoka Kabwe na kuthibitishwa na polisi mkoani hapa, zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 6, saa
11 jioni katika maeneo ya Kijiji cha Mkombe wakati boti hiyo ilipokuwa ikisafari kutoka Kijiji cha Kabwe kuelekea Kijiji cha Kalila kilichopo Mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage aliwataja waliofariki maji katika ajali hiyo kuwa ni Emmanuel Makasi (1) Mkazi wa Tunduma, Helena White (1) Mkazi wa Kabwe, Korodina Tende (1), Modesta Mengo (6)
na Apolinali Roman maarufu Sungura (36) wote wakazi wa kijiji cha Kalila.

Kamanda huyo alisema kuwa watu 21 waliokolewa kutokana na jitihada za
wavuvi walikuwepo maeneo ya karibu ambapo wanne hawajulikani walipo na wanahofiwa kufa maji baada ya kuzama kwa boti hiyo.

Mmoja wa manusura ajali hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mbunge Ramadhani alisema ajali hiyo
ilitokea baada ya boti hiyo mali ya mfanyabiashara aliyefahamika kwa
jina moja la Charles yenye jina la usajili Kasongo ya Mizimu kupasuka
na kuzama ikiwa safari kuelekea kijiji cha Kalila.

Aliongeza kuwa wakati wakiwa safarini ghafla boti hiyo inayokadiriwa
kuwa na watu wapatao 36 ikiwa na mizigo ilipasuka na kuanza kuzama
ambapo baadhi ya watu walifanikiwa kuogelea hadi ufukweni na kuokoa
maisha yao.

“Ilikuwa ajali mbaya, Mungu ametusadia sana wengine , mimi nilishikilia mbao za ile boti mpaka nilipopata msaada kutoka kwa wavuvi walikuwa maeneo ya jirani na kutuokoa baadhi yetu hadi nchi kavu huku wengine wakihofiwa kufa, tulikuwa wengi zaidi ya 36,” alisema Ramadhani.

Kwa mijibu wa Kamanda Mantage, polisi wilaya Nkasi kwa kushirikiana
wananchi wanaendelea kutafuta miili mingine ya watu wanahofiwa kufa maji kwenye ajali hiyo, huku akitoa rai kwa wavuvi na wananchi wengine wa vijiji vya jirani kutoa taarifa iwapo miili ya watu hao itaonekana ikielea majini.

No comments: