
Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal amewataka watumishi wa ofisi ya Makamu wa Rais kujizatiti katika utekelezaji wa majukumu yao ili waweze kupata mafanikio zaidi katika awamu hii ya pili ya uongozi wa Rais Kikwete.
Akizungumza na Menejimenti ya ofisi hiyo Dk. Bilal alisisitiza umuhimu wa watendaji na watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba, sheria pamoja na kuzingatia taratibu za mawasiliano ya kiserikali.
Aliwakumbusha watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kama timu moja, ya serikali moja, na nchi moja na kueleza matumaini yake kuwa watumishi hao watajituma kwa kuzingatia utawala bora, uwazi na kuendeleza heshima ya ofisi.
Aidha, Dk. Bilal alisema majukumu ya wizara mbili katika ofisi hiyo yaani za Muungano na Mazingira ni muhimu sana kwa mustakabli wa taifa na hivyo hawana budi kuwa makini katika utekelezaji wake huku wakizingatia ujuzi wao, taaluma na uzoefu wao.
Aliwakumbusha watumishi wa ofisi hiyo wajibu wao wa kuelewa mfumo mzima wa utendaji wa serikali ili aweze kufanikisha majukumu yake ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Bibi Ruth Mollel aliahidi kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu, sheria na utawala bora kama alivyoelekeza na kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010.
No comments:
Post a Comment