.jpg)
Tume ya Uchaguzi ya Taifa leo itaendelea kutangaza matokeo ya Urais wa Tanzania, baada ya kusitisha shughuli hiyo hapo jana ikiwa tayari imeshatangaza matokeo ya nafasi ya Urais kwa majimbo mia moja kumi na sita.
Matokeo kwa majimbo hayo yamekuwa yakitangazwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Lewis Makame na Makamu mwenyekiti wake Jaji Omar Makungu ambapo yamebakia matokeo kutoka majimbo 123, huku mwelekeo ukionyesha kuwa mgombea urais kupitia CCM Dokta Jakaya Kikwete anaongoza katika majimbo mengi.
Kwa upande wa ubunge, hadi sasa tume imeshatangaza matokeo katika majimbo 113, ambapo CCM inaongoza ikiwa na viti 73, ikifuatia na CHADEMA yenye majimbo 20, CUF majimbo 15, NCCR-MAGEUZI viti Vitatu na TLP viti viwili vya ubunge.
Wakati huo huo, kitendawili cha nani ataibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha ubunge kwenye majimbo matatu yaliyoko manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, kimeteguliwa usiku wa kuamkia leo baada ya Msimamizi wa uchaguzi wa manispaa hiyo Gabriel Fuime kuwatangaza wagombea kupitia CCM katika majimbo hayo kuwa ni washindi.
Wabunge hao wateule ni Makongoro Mahanga kwa jimbo la Segerea, Eugenie Mwaiposa kwa jimbo la Ukonga huku Mussa Azan Zungu akitetea jimbo la Ilala.
Kwa takribani siku nne, ofisi za Arnatoglou zilikuwa kambi ya majumuisho ya kura kwa ajili ya viti vya ubunge vya majimbo ya Ilala, Segerea na Ukonga ambayo yote yako katika manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Na jimbo la Rombo limenyakuliwa na CHADEMA baada ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo Samuel Kibaja kumtangaza mgombea wa chama hicho, Joseph Selasini kuwa mshindi.
Hata hivyo, Mwakilishi wa mgombea wa CCM, Basil Mramba aliripotiwa kukataa kutia saini matokeo hayo kwa madai kuwa matokeo yalicheleweshwa kufikishwa kwenye vituo na hivyo wameomba kupatiwa nakala ya kila kituo ili waweze kulinganisha na matokeo waliyonayo.
No comments:
Post a Comment