Wednesday, October 20, 2010

Wazo la Joseph Kulangwa......

KAMPENI zinaendelea kwa wagombea kujinadi katika hatua hizi za mwishomwisho katika juhudi za kuomba ridhaa ya wananchi wawachague kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, huku ndimi tamutamu zikitolewa.

Wagombea wanapata fursa ya kupanda majukwaani na kujinadi kwa sera zao, ingawa kunakuwapo tofauti za wanaonadi sera zao lakini wapo wanaojinadi kwa kuponda sera za wenzao na pia kuwaponda washindani wenzao.

Mimi nadhani ni bora zaidi kunadi sera zako ukiwaambia wananchi ukiingia madarakani utafanya nini, badala ya kupanda jukwaani kumponda mwenzako na hata kumvurumishia matusi kana kwamba si binadamu mwenye hisia.

Pengine ukosefu wa sera ndio unaosababisha hayo na hata sehemu zingine watu kushikana na kutiana ngeu pasipo na sababu ya msingi ya kufanya hivyo na hata kampeni sasa kuonekana ni ulingo wa masumbwi na si sera tena.

Ingawa kampeni ni sawa na mwamba ngoma, ngozi kuvutia kwake, lakini hakuna sehemu au kanuni ya kampeni inayoelekeza kuwa hata kama kuna jema amelifanya mshindani wako, basi ponda tu huku ukweli ukiwa ni dhahiri.

Pengine ni bora kama mgombea anaona kwamba mwenzake ana zuri alilolifanya ambalo ni silaha yake kisiasa, basi asilitaje, bali anyamaze na kuumia nalo moyoni, kwani wanasema palipo na ukweli uongo sharti ujitenge.

Hivyo zuri ni zuri hata likitajwa kwa ubaya, litaendelea kuwa zuri tu daima. Kwa kuwa ulimi ulimponza kichwa, ndiyo sababu ni vema kama mtu anadhani anachokisema hakina uhakika au kina ukweli wa kisiasa, anyamaze nacho tu.

Hivi karibuni akiwa Chato mkoani Kagera, mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari, akimponda Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli, kuhusu uchomaji nyavu.

Mgombea huyo akasema kitendo cha wavuvi kuchomewa nyavu zao ni unafiki na uonevu! Akisema badala ya nyavu hizo kuchomwa, viwanda vinavyozitengeneza ndivyo vingedhibitiwa badala ya kuzichoma baada ya wavuvi kudunduliza fedha na kuzinunua.

Bila shaka daktari huyu anaelewa ni nini maana ya mazalia ya samaki na anaelewa kwa nini nyavu za matundu madogo ni hatari kwa mazalia na makuzi ya samaki, na anaelewa kuwa kauli yake hiyo ni ya kisiasa na haina ukweli wa dhati.

Mimi nadhani angekuwa mtenda haki kama angepongeza hatua za Magufuli, lakini akaendelea kutaka viwanda vidhibitiwe visizalishe nyavu hizo tena; lakini hapa anatwambia kuwa viwanda vidhibitiwe, lakini uvuvi kwa nyavu za matundu madogo uendelee, mpaka zitakapochakaa.

Hii ni sawa na kusema mashamba ya bangi yasichomwe moto, lakini majembe yanayotumiwa kulimia mashamba hayo ndiyo yazuiwe au kwamba watoto wetu waendelee kubwia ‘unga’, ila mkazo uwe katika kuzuia dawa hizo kuingia nchini.

Kuna usemi, kwamba mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, aliyoyafanya Magufuli ni makubwa katika wizara nyingi alizopewa kutumikia kwa miaka yote ya uongozi wake, hilo Dk Slaa analijua ila anatumia siasa kupindisha ukweli.

Ni wazi kuwa wananchi wa Chato wanamfahamu Magufuli, sina nia ya kumpigia kampeni, lakini mafuta daima huelea kwenye maji, tuendeshe kampeni zinazowaambia wananchi ukweli, huku tukichelea kuwafanya wananchi hao ambao ndio wapiga kura, mbumbumbu wasiojua chochote.

Hii inamfanya mwananchi ajiulize, kama Dk Slaa atapewa ridhaa na wananchi kuongoza nchi hii, ataruhusu uvuvi wa kutumia nyavu zenye matundu madogo?

Bila shaka jibu ni hapana, ila anatumia jukwaa hili kama njia ya kuingilia Ikulu na akifika huko ndipo ataona uhalisia wa mambo na atamuunga mkono Magufuli.

Tujifunze kuona mema yaliyofanywa na kambi tofauti, mathalani kama Serikali ya CCM imefanya mazuri basi yasemwe bila kigugumizi wala kupindisha ulimi na kama kuna mazuri ya wapinzani nayo yasemwe vivyo hivyo, kwani hatimaye nchi hii ni yetu.

Tusitake kujidanganya wenyewe huku tukipindisha mambo ambayo baadaye yatatusuta. Tuzingatie kauli ya mgombea ubunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe, kwamba kuna maisha pia baada ya uchaguzi.

No comments: