
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, amekacha kuzungumzia uamuzi alioutoa juu ya pingamizi lililowasilishwa kwake na Chadema dhidi ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Jana Tendwa alikiri kumaliza kulishughulikia pingamizi hilo na kulitolea uamuzi, lakini akasema hawezi kuwaeleza waandishi wa habari alichoamua.
Septemba Mosi mwaka huu Chadema iliwasilisha pingamizi hilo kwa Msajili wa vyama vya siasa kumtaka amwondoe Kikwete kwenye kinyang'anyiro cha urais kwa madai kuwa amekiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi wakati wa kampeni zake.
Chadema ilimshutumu Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake, kutangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi na kuahidi kulipa madeni ya vyama vya ushirika wakati wa kampeni.
Kwa mujibu wa Chadema, vitendo hivyo ni rushwa kulingana na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 kwa kuwa vinashawashawishi wapigakura wamchague katika uchaguzi ujao.
Baada ya kulipitia pingamizi hilo, Tendwa alitolea uamuzi, lakini jana alipotakiwa kueleza uamuzi aliotoa alijibu,"Sheria inaniagiza nikishafanya uamuzi niwape wahusika. Mimi sina madaraka ya kusema hayo."
Aliongeza: "Mimi nadhani kwa sasa (CCM na Chadema) wanatafakari nilichoamua. Mimi nitaweza kusema chochote baada ya wao kuzungumza, labda wakilalamika ndipo nitatoa ufafanuzi.”
Wakati Tendwa akikataa kuelezea uamuzi wake, CCM iliweka wazi kuwa Msajili huyo wa ametupilia mbali pingamizi hilo la chadema kwa maelezo kuwa madai yao hayana msingi.
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alisema jana kuwa Chadema wanapaswa kujifunza na siyo kutaka kujipatia umaarufu kwa jambo lisilo la msingi.
Makamba alitamba kuwa hiyo ni rasharasha na kwamba, Chadema watarajie gharika ya kimbunga Oktoba 31, mwaka huu wakati Watanzania watakapomiminika vituoni na kuichagua CCM kwa kishindo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni za mgombea urais wa CCM, Abdulrahman Kinana, alifafanua kuwa hukumu hiyo ina vipengele vitatu.
Kinana alieleza kuwa Tendwa ametupa pingamizi hilo kwa sababu halina msingi na kwamba, malalamiko hayo yameleta bugudha kwa wananchi, mgombea na wanachama wa vyama vyote viwili.
"Msajili anasema malalamiko hayo yameamsha chuki baina ya wanachama wa vyama vyote viwili na wananchi kwa ujumla pamoja na kumsababisha bughudha kwa wanachama na mgombea," alisema Kinana akisoma uamuzi wa Tendwa.
Kinana anaeleza kuwa katika kipengele cha tatu cha hukumu hiyo Msajili ameielimisha Chadema kwamba, katika kampeni wagombea wanawajibika kujikita katika sera, programu na kazi walizofanya au kukusudia kufanya.
"Kwa sababu hiyo, Tendwa amebaini kuwa pingamizi la Chadema limejaa tuhuma ambazo hazijathibitishwa," alisema Kinana na kuongeza:
"Tuhuma kama hizi ni lazima ziepukwe ili kuondoa migongano".
Kinana alifahamisha kuwa suala la mgombea wa CCM kutangaza mishahara ya wafanyakazi na kuahidi kulipa madeni ya vyama vya ushirika ili visifilisike, ni programu ya kisera ya chama hicho ambayo ni halali kuelezwa hadharani kipindi hiki cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Chadema jana walikataa kuzungumzia uamuzi uliotolewa dhidi ya pingamizi lao kwa maelezo kuwa wanawasubiri wanasheria wa chama hicho kuifungua barua hiyo, kuisoma na kisha kutolea tamko lao.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliliambia Mwananchi kuwa barua waliyotumiwa na Tendwa ina muhuri wa siri wa serikali unaokataza kusambazwa kwa watu hivyo hawezi kueleza kilichoandikwa ndani yake.
“Ni kweli tumepokea majibu ya malalamiko yetu toka kwa msajili wa vyama vya siasa leo asubuhi, lakini yana chapa ya mhuri wa siri wa serikali. Kwa msingi huo sisi hatuwezi kutoa majibu labda mumfuate yeye mwenyewe,” alisema Mnyika
Katika madai ya Chadema, licha ya kumtuhumu Kikwete kuongeza mishahara kinyemela, wanamlalalmikia kuhusu ahadi yake ya kukilipia deni la Sh5 bilioni Chama cha Ushirika cha Nyanza.
Mambo mengine waliyolalamikia ni ahadi ya kununua meli mpya kubwa kwa ajili ya usafiri wa Ziwa Victoria na kutoa ahadi nyingi zilizo nje ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM
CCM iliwasilisha utetezi kuhusu pingamizi la Chedema ikimtaka msajili atupilie mbali pingamizi hilo kwa maelezo kuwa alichofanya mwenyekiti wao si kutangaza mishahara jukwaani bali alitoa ufafanuzi wa namna serikali yake kwa kipindi cha miaka mitano ilivyokuwa ikiboresha mishahara ya wafanyakazi.
Kuhusu ahadi ya kulipa Sh.5 bilioni, CCM ilisema Kikwete alikuwa akinadi sera za chama hicho ambazo zimo kwenye ilani ya uchaguzi, zinazoeleza namna ya kuimarisha vyama vya ushirika na kuahidi serikali yake kulipa madeni ya vyama vya ushirika.
Imeandaliwa na Leon Bahati na Fredy Azzah
No comments:
Post a Comment