Thursday, December 30, 2010

Chengeeeeeeeeeeeeee...vijisentiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Kivukoni-Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemtia hatiani Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kwa kumtaka kwenda jela miaka mitatu au alipe faini ya Sh700,000, kwa kosa la matumizi mabaya ya barabara na kusababisha vifo vya watu wawili.

Chenge ambaye ni Mwansheria Mkuu wa Serikali wa zamani na Waziri katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, alitiwa hatiani jana katika hukumu iliyosomwa mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kwey Rusema. Hata hivyo, alifanikiwa kulipa faini hiyo, hivyo kuachiwa huru.

Awali hukumu dhidi ya kiongozi huyo ilikuwa isomwe Desemba 16, mwaka huu, lakini iliahirishwa hadi jana kutokana na kile ambacho hakimu Rusema alisema kuwa ni Chenge kuwa safarini jijini Mwanza alikoenda kuhudhuria msiba.

Hatimaye kesi hiyo ilifikia tamati yake rasmi jana baada ya machakato wa kusikilizwa kwake uliochukua karibu miaka miwili kukamilika.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba Machi 27 mwaka 2009 katika makutano ya barabara ya Haileselasie na Ali Hassan Mwinyi eneo la Morogoro Store jijini Dar es Salaam, Chenge aliigonga bajaji na kuwaua wasichana wawili waliokuwa abiria kwenye bajaji hiyo; Beatrice Constantine na Victoria George. Kesi hiyo ilifunguliwa mahakama hapo kwa mara ya kwanza Machi 31 mwaka 2009 na kuanza kusikilizwa mwezi Aprili mwaka 2010.

Katika kesi hiyo, Chenge alishtakiwa kwa makosa manne; kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha vifo vya watu wawili, kuharibu mali na kuendesha gari isiyokuwa na bima. Akitoa hukumu ya kesi hiyo jana, hakimu Rusema alisema mahakama imeona Chenge ana hatia katika makosa yote manne na hivyo kumtoza faini ya Sh700,000 ama kifungo cha miaka mitatu jela. "Katika kosa la kwanza na la pili, mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh 250,000 kwa kila kosa au kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kila kosa hilo," alisema Hakimu Rusema.

Aliongeza "Katika kosa la tatu na kosa la nne, mshtakiwa atalipa Sh 100,000 kwa kila kosa au kifungo cha miezi 6 kwa kila kosa hilo. Hivyo, atatakiwa kulipa jumla ya Sh 700,000 kwa makosa yote au kwenda jela miaka mitatu." Kabla ya kusoma hukumu hiyo hakimu Rusema alimpa Chenge ambaye alikuwapo mahakamani hapo nafasi ya kujitetea, lakini badala yake alisimama wakili wake.

Akitoa utetezi wa mtuhumiwa huyo wakili Senen Mponda alisema," Hili ni kosa la kwanza kwa mshtakiwa. Mshtakiwa ni kiongozi wa umma na kuhusu bima ilikuwa bahati mbaya." "Naomba apunguziwe adhabu ili apate kuendelea na shughuli zake za kuutumikia umma." Awali ilielezwa mahakamani hapo kuwa Machi 27 mwaka 2009 kati ya saa 8.15 na 8.30 usiku katika eneo la Oyesterbay, makutano ya barabara ya Haile Selasie na Ally Hassan Mwinyi, Chenge akiwa anandesha gari binafsi aliigonga bajaji hiyo na kusababisha vifo vya watu wawili.

Ilielezwa kuwa Chenge aliigonja bajaji hiyo akiwa na gari aina ya Toyota Hillux Double Cabin wakati akirudi nyumbani kwake akitokea klabu ya British Legion akiwa kwenye mwendo wa kati ya ya kilomita 70 hadi 100 kwa saa.

No comments: