
KILIO cha muda mrefu cha wanafunzi wa elimu ya juu nchini kuhusu mikopo kinaelekea kufikia ukingoni baada ya mkuu wa nchi kuingilia kati.
Rais Jakaya Kikwete jana alitangaza kwamba ataunda Tume Maalumu ya kuchunguza mfumo mzima wa utoaji mikopo hiyo kwa wanafunzi hao.
Lakini pia alisema ataangalia utendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi hao kwa nia ya kuboresha mfumo uliopo na kuleta ufanisi zaidi.
Katika kuonesha dhamira yake ya dhati, Rais alisema Tume hiyo ifikapo Januari mwakani, itakuwa imeundwa na ataiagiza ikusanye mawazo kwa wamiliki wa vyuo vikuu, wahadhiri na wanafunzi.
Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo jana, alipofungua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kingine chochote nchini na ambacho kimejengwa kwa miaka minne ya kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Kikwete.
Huku akishangiliwa na wanafunzi waliojazana katika ukumbi wa Chimwaga ulioko chuoni hapo, Rais Kikwete aliwaambia mamia ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo:
“Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo, ili wanafunzi wengi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni.”
Aliongeza: “Serikali imeongeza fedha za mikopo ya wanafunzi kutoka Sh bilioni 56.1 mwaka 2005/06 hadi Sh bilioni 237 mwaka 2010/11.
Wanafunzi waliopewa mikopo, wameongezeka kutoka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi.”
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itatoa maelekezo mahsusi wakati hatua hiyo ikitekelezwa.
Kuhusu mchango wa sekta binafsi katika elimu nchini, Rais Kikwete alitoa mwito kwa sekta hiyo nayo kupanua vyuo vikuu ilivyonavyo sasa na kujenga vipya.
“Wamefanya kazi nzuri ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika eneo hili lakini bado mahitaji ni makubwa kuliko uwezo uliopo sasa. Tuuongeze. Sisi katika Serikali tutaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji wa sekta binafsi katika elimu ya juu.
“Pia, tutaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi kama tufanyavyo sasa. Ombi langu kwao wasipandishe sana ada, kwani watawakwaza wazazi na wanafunzi kwa kile kiasi ambacho itawabidi walipe wenyewe zaidi ya mkopo unaotolewa na Serikali.”
Alisema uzinduzi wa UDOM ni mwanzo wa safari ndefu ya kukijenga na kufikia kiwango cha juu kinachotarajiwa na wote.
“Safari yoyote haikosi changamoto zake, lakini napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo kuzikabili changamoto zilizopo na zitakazojitokeza siku za usoni. Maombi yangu kwa uongozi wa jumuiya ya chuo hiki ni kwanza, muitunze na kuitumia vizuri miundombinu hii ili idumu.
“Wahenga walisema ‘kitunze kikutunze’. Pili, mwongeze bidii na maarifa katika kutambua na kutafuta majawabu kwa vikwazo vinavyojitokeza. Yaliyo juu ya uwezo tupo tutasaidiana,” aliahidi Rais Kikwete.
Awali katika hotuba yake, Rais Kikwete alikiri kuwa alisema suala la kujenga chuo kikuu kipya kwa woga wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.
“Lakini niliamua kulifuatilia kwa nguvu mara baada ya kuchaguliwa, kwani ahadi ni deni. Sina budi kutoa shukrani maalumu kwa Profesa Peter Msolla aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu wakati ule na Profesa Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa mawazo ya awali na ushauri wao kuhusu ujenzi wa chuo hiki. Mawazo yao ndio msingi tulioutumia kuanza kazi iliyotufikisha hapa tulipo sasa,” alisema Rais Kikwete.
Aidha, alimshukuru Rais mstaafu Mkapa kwa kukubali ombi la kuwa Mkuu wa Chuo hicho, akisema asingeshangaa wala kukasirika kama angemwomba radhi na kumshauri atafute mtu mwingine, ili apate nafasi ya kufurahia kustaafu kwake baada ya miaka 10 ya kazi ngumu ya kuongoza Taifa.
“Nakushukuru na kukupongeza sana wewe, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Makamu wa Rais Dk. Mohamed Ghalib Bilal, wajumbe wa Baraza la Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Idris Kikula na naibu wako wawili kwa kazi kubwa na nzuri mliyofanya katika ujenzi wa chuo hiki,” aliongeza.
Rais aliupongeza pia uongozi wa UDOM kwa kutimiza ndoto yake na akautaka kukitunza chuo hicho ambacho ni moja ya vyuo vizuri zaidi Afrika.
Tume hiyo itakapokuwa imeanza kazi, bila shaka itaondoa kelele nyingi kuhusu mikopo ambazo zingine zilikuwa zikitumika kisiasa na baadhi ya wanasiasa na kusababisha wanafunzi kutofuatilia masomo yao.
UDOM ilizaliwa kutokana na wazo binafsi la Rais Kikwete katika kutafsiri maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi wa CCM mwaka 2005 iliyotaka kupanuliwa kwa fursa katika elimu ya juu.
Pamoja na Rais Kikwete kwenye sherehe hizo, wengine waliohudhuria walikuwa ni Rais Mkapa, Dk. Bilal, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Chuo hicho na Makamu Mkuu wake, Dk. Kikula.
Dk. Bilal pia alikuwa Mhadhiri wa Fizikia na Msimamizi wa Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika chuo hicho.
No comments:
Post a Comment