Mbeya,
leo kumekuwa na mgomo wa daladala za kutoka Uyole kuelekea Sokomatola.
Mgomo wenyewe umetokana na sababu za kijinga kijinga tu ukizisikia.
Kwamba kwakuwa wameambiwa wabadili njia pale maeneo ya Soweto ili
kuepusha msongamano hasa nyakati za asubuhi na jioni basi wapewe idhini
ya kupandisha nauli ifike shs 500.
Nasema ni ujinga kwasababu, mara kadhaa nimepanda daladala na zikapita maeneo hayo
na nikawasikia madereva na makonda wakisema kuwa inawapa mwanya wa
kupata abiria hususan nyakati za mchana na jioni kwani kuna wanaoenda
kuwaona wagonjwa, na pia kupata abiria wa sokoni pale Soweto kwa wingi.
Kwahiyo kwa upande mmoja mabadiliko hayo yamewanufaisha sana tu.
Lakini pia, mabadiliko haya hayajaongeza urefu wa safari kwa kiwango
cha kuwafanya wadai kuwa wanapata hasara. Kwa wanaokaa Mbeya watakuwa
wanaelewa hili. Sasa haya madai ya waongeze nauli yanaletwa na nini
hasa?
Na ikumbukwe kuwa hata viwango vya sasa vya nauli
walipandisha kwa mgomo wakati mafuta yamepanda bei kwa shilingi
zisizofikia 100. Lakini yaliposhuka hawakushusha viwango hivyo vya
nauli. Na iliwahi hojiwa, inakuwajr mafuta yakipanda wanadai kipandisha
nauli tena wanaongea huku mapovu yakiwatoka midomoni lakini yanaposhuka
hawashushi?
Kiukweli kabisa, ili kudhibiti hali hii,
ningemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kwa kushirikiana na SUMATRA, wafute
leseni za wote waliogoma na kutangaza kutoa upya leseni kwa ruti hiyo na
zingine zitakazoleta shida, kwa wale ambao watakuwa tayari kufuata
taratibu ambazo zinakuwa na manufaa kwa watoa huduma na wahudumiwa pia.
Tukiendekeza kukinga mikono kwa hawa mabwana kila wanapokohoa na
kuwaambia wateme tu mate yao tutakinga kwakuwa tunawapenda na
kuwathamini sana, iko siku watazusha makubwa zaidi na vilio kwetu
vitakuwa vikubwa zaidi.
Hatuwezi kuishi humu nchini kama tuko
kwenye bwawa la kambale. Kila mmoja ana sharubu kwahiyo anajiona mkubwa
na anaweza amua anachotaka yeye. Ujinga mtupu.
Rama Msangi,
Kalobe, Mbeya
No comments:
Post a Comment